Friday, October 2, 2009

Sanduku la kupigia kura.

Baadhi ya wagombea wanaowania nafasi mbalimbali katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa Jijini Dar es Salaam, wameanza kutoa ahadi mbalimbali kwa wananchi ili waweze kupigiwa kura.
Mgombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Ndumbwi uliopo Mbezi Juu, kupitia CCM, Bw. Salustian Kashimiry Kimaro almaarufu kwa jina la Kim, amesema endapo atachaguliwa atamaliza tatizo sugu la ukosefu wa maji katika mtaa huo.
Amesema tatizo la maji katika mtaa huo ndilo linalomnyima usingizi, na kwamba endapo atapewa ridhaa ya kuongoza, ndilo litakuwa la kwanza kuvaliwa njuga.
Bw. Kimaro ambaye katika kura za maoni alimbwaga vibaya aliyekuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Bw. Oswald Mwasuka, ametoa ahadi hiyo wakati akichukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.
Amesema atahakikisha anashirikiana na Serikali Kuu kutatua tatizo hilo ambalo limekuwa kero kwa wakazi wa mtaa huo.
"Nia ninayo na uwezo ninao wa kuhakikisha maji yanapatikana haraka katika mtaa wangu wa Ndumbwi nitakapoingia madarakani," akasema Bw. Kimaro mbele ya wananchi kibao wa mtaa huo ambao walijitokeza kumsindikiza kwenda kuchukua fomu ya kugombea.
Ameongeza kuwa mbali ya kero hiyo pia atahakikisha anashughulikia suala la ulinzi kutokana na hali ya sasa ya kiusalama kuwa mbaya.
Bw. Kimaro amesema mbali ya kero hizo pia atashughulikia tatizo la Mto Ndumbwi ambao nyakati za mvua haupitiki na kusababisha kero kwa wananchi.
Mgombea mwingine wa nafasi ya Uenyekiti katika mtaa wa Jogoo kupitia CCM, Bw. Juma Mnaka amesema endapo atachaguliwa kuongoza mtaa huo, atahakikisha anashughulikia matatizo kibao yanayoukumba mtaa huo likiwemo la barabara mbovu na uchafuzi wa mazingira.

No comments:

Post a Comment